SEHEMU A: SARUFI
Andika herufi ya jibu sahihi
Urefu wake ulifanya acheze vizuri mpira wa kikapu. Neno urefu limetumika kama
(a) nomino (b) kielezi (c) kivumishi (d) kihisishi (e) kiwakilishi
Juma anacheza mpira. Hii ni kauli ya ________________
(a) kutenda (b) kutendwa (c) kutendewa (d) kitendo (e) kutendana
Katika neno “watasoma” kiambishi kinachoonesha nafsi ni kipi?
(a) –ta - (b) wa - (c) –so- (d) – ma (e) –tas -
“Vidani hivi vimenunuliwa.” Sentensi hii ipo katika wakati gani? _______
(a) desturi (b) uliopita (c) uliopo (d) ujao (e) mtimilifu
Umoja wa sentensi “Kucha zangu zimekatika” ni upi?
(a) Kucha yangu imekatika (b) Ukucha wangu umekatika
(c) Ukucha wako umekatika (d) Kucha imekatika
(e) Kucha zangu imekatika
Kauli taarifa ya sentensi isemayo “Nataka Helena ajibu swali hili upesi” ni ipi? __
(a) Alitaka Helena ajibu swali lile upesi (b) Helena alitaka ajibu swali upesi
(c) Helena alisema namtaka ajibu swali lile (d) Alitaka Helena aulize swali upesi
(d) Helena jibu swali lile upesi
Mariamu angelia kwa sauti _______ msaada.
(a) angelipata (b) angepata (c) angalipata (d) angapata (e) angeripata
Kinyume cha neno ughaibuni ni kipi?
(a) nchi za jirani (b) magharibi (c) nchi za mbali (d) mashariki (e) nchi za nje
Mtoto huyu alikuwa na bidii darasani __________ hakufaulu mtihani.
(a) hivyo (b) hata hivyo (c) angalau (d) aghalabu (e) mintarafu
Hakuna mtu _______ aliyetaka kufahamu masuala hayo.
(a) yoyote (b) wowote (c) yeyote (d) mmoja (e) hata
Neno NGISI lina konsonanti ngapi? ______________
(a) moja (b) mbili (c) tatu (d) nne (e) tano
Kuna irabu ngapi kwenye neno SABASABA? ______________
(a) nne (b) nane (c) nyingi (d) chache (e) moja
Maneno “mrefu, mweusi, mwerevu na mpole” yakitumika pamoja na majina hufanya kazi gani?
(a) kivumishi (b) kielezi (c) kitenzi (d) nomino (e) kiwakilishi
Nyimbo _____ ni nzuri
(a) zetu (b) yetu (c) yao (d) yenu (e) yake
Nomino michezo inatokana na kitenzi ______________
(a) mchezaji (b) chezo (c) cheza (d) kucheza (e) mchezo
SEHEMU B: MISAMIATI
Andika herufi ya jibu sahihi au fuata maelekezo ya swali pasipokuwa na machaguo
Wewe utazungumza kwa ___________ ya mwalimu mkuu
(a) njia (b) niaba (c) mara (d) sababu (e) badala
Nimetuma ujumbe lakini sijapata mrejesho wowote. Neno lililopigiwa mstari lina maana sawa na neno lipi?
(a) asante (b) ushauri (c) mwaliko (d) jibu (e) mawasiliano
Ng’ombe dume aliyehasiwa ambaye hutumika kwa kufanya kazi kama vile kuvuta mkokoteni au kukokota plau huitwa ___________
(a) mbuguma (b) beberu (c) maksai (d) gegedu (e) fahali
Mawaidha ni ______________
(a) wosia (b) maono (c) ushauri (d) maradhi (e) hotuba
Kutembea kwa matao ni kutembea kwa mwendo wa _________
(a) kasuku (b) maringo (c) polepole (d) haraka haraka (e) kuchechemea
Mzee yule ana kibiongo. Kibiongo ni ______________
(a) nundu (b) pua kubwa (c) jicho moja (d) mfupi (e) toinyo
Kinyume cha neno HASIMU ni ___________
(a) adui (b) rafiki (c) ghadhabu (d) aghalabu (e) mzazi
Mtu anayesaliti nchi au serikali huitwa _____________
(a) haini (b) fedhuli (c) mzalendo (d) kaidi (e) fisadi
Wanafunzi wote walipoelezwa walielewa isipokuwa Tino ambaye ni ________
(a) Bilula (b) Renge (c) Damisi (d) Gomesi (e) Luja
Msichana yule ana nywele za __________
(a) singa (b) katani (c) mafuta (d) mnato (e) marashi
SEHEMU C: METHALI, NAHAU NA VITENDAWILI
Andika herufi ya jibu sahihi au fuata maelekezo ya swali pasipokuwa na machaguo
Kamilisha methali ifuatayo. “Mwacha asili ni ____________
(a) mjinga (b) mtumwa (c) mgeni (d) mtalii (e) mzalendo
Tegua kitendawili kifuatacho. “Kondoo wetu ana ngozi ndani na nyama nje. ____
Dalili ya mvua ni mawingu. Methali nyingine yenye maana sawa na hiyo ni ____
(a) Debe shinda haliachi kutika (b) Mtegemea nundu haachi kunona
(c) Mwanzo wa ngoma ni lele (d) Ukistaajabu ya Musa utaona ya Firauni
(e) Mbio za sakafuni huishia ukingoni
Heri kufa macho kuliko ______________
(a) kufa mwili (b) kufa moyo (c) kufariki dunia
(d) kufa masikio (e) kufa mdomo
Manahodha wengi chombo huenda mrama. Ni methali gani kati ya hizi zifuatazo inapingana na hii? ___________
(a) Kwenye watu wengi haliharibiki neno (b) Jungu kuu halikosi ukoko
(d) Mchimba kisima huingia mwenyewe (d) wingi si hoja (e) Wengi wape
Tegua kitendawili kifuatacho. Ajihami bila silaha. ____________
Jibu la kitendawili: “Nikimpiga mwanangu nalia mwenyewe” ni ________
Maana ya nahau “kupiga chuku” ni ipi? __________
(a) kutoa maneno machafu (b) kutoa maelezo ya uongo
(c) kuchukia jambo fulani (d) kusema ukweli (e) kutunza siri
Meli ilitia nanga baharini. “Kutia nanga” maana yake ni ____________
(a) kuondoka (b) kuelea (c) kwenda kasi
(d) kusimama (e) kwenda polepole
Samahani ndugu umenitoka. Maana ya neno umenitoka ni ipi? ___________
(a) umeniacha (b) umenikimbia (c) nimekusahau
(d) umenichoka (e) umenifia
SEHEMU D: UFAHAMU
Soma habari ifuatayo kwa makini kisha jibu swali la 36 – 45
Mashitaka yaliyomkuta Mzee Mkenule hayakuwa ya kawaida na yalivuta umati mkubwa wa watu.
Siku ya hukumu ndiyo usiseme hapakuwa hata na sehemu ya kutema mate. Miji yote kadhalika haikuwa na habari nyingine isipokuwa mashtaka yaliyomkabili Mheshimiwa Mzee Mkenule na majaaliwa yake siku hiyo ya hukumu. Hata maduka yaliyo maarufu maeneo ya miji yalikosa washitiri.
Jaji naye siku hiyo alikuwa na muonekano tofauti, wazee wa baraza walikuwa kama wengine. Haikujulikana mara moja kama ni uzito wa shauri lile, wingi wa watu au macho ya watu yalipatwa na ukungu hata wayatazame mambo kinyume cha yalivyo.
Upande wa mawakili, wataalamu wa sheria wanaojua kupingana kwa vifungu vya sheria katika mambo yote, maana kwao hakuna dogo, rangi nyeupe yaweza kuwa nyekundu au njano kuwa nyeusi ili mradi sheria imetumika kuhalalisha mwanasheria anachosimamia. Nao pia hali ilikuwa nyingine siku hiyo. Wote walivalia suti nyeusi kifuani kuking’ara mashati meupe pee, kana kwamba yametoka kiwandani maalumu kwa ajili hiyo.
Baada ya mabishano makubwa ya wanasheria juu ya shauri linalomkabili mzee Mkenule, hatimaye ilikuwa ni zamu ya jaji kutoa hukumu.
Hukumu ilisomwa kwa muda mrefu, yapata masaa matatu. Jaji alianza na usuli wa kesi yenyewe, kisha mwenendo wa kesi. Hatimaye alihitimisha kwa kumuondolea mashtaka ya Uhaini Mheshimiwa Mkenule kosa ambalo kama angepatikana na hatia angetupwa lupango kwa miaka isiyopungua ishirini na kenda.
MASWALI
Mashitaka yaliyomkabili Mzee Mkenule yalihusu __________
(a) ujangili (b) uhaini (c) uheshimiwa (d) uanasheria (e) uwakili
Neno gani limetumika badala ya sentensi “historia ya mashitaka” kwenye habari uliyosoma?
(a) mwenendo (b) mashtaka (c) shauri (d) usuli (e) kenda
Neno “kenda” lina maana sawa na ________
(a) tisa (b) tano (c) kumi (d) ishirini (e) muongo
Mawakili hubishana katika mambo kwa vifungu vya sheria kwa kuwa ________
(a) hawajui sheria (b) ni wabishi (c) ni weledi wa sheria
(d) basi tu (e) wanavaa suti nyeusi
Ni nani alikuwa akikabiliwa na mashtaka?
(a) Mzee Mkenule (b) Jaji (c) usuli (d) wazee wa baraza (e) wakili
Neno gani limetumika badala ya jela? _______________
Nani alitumia muda mrefu kuzungumza siku ya hukumu? ____________
“Hapakuwa hata na sehemu ya kutema mate.” Maana yake ni _________
(a) usafi wa mazingira (b) wingi wa watu (c) kote kulijaa mate
(d) sehemu yote ni chafu (e) sehemu yote ilikuwa kavu
Kichwa cha habari hii kingefaa kuwa _______________
(a) mashtaka (b) mashtaka ya Mzee Mkenule (c) Hofu
(d) Siku ya Kiyama (e) Kuondolewa mashtaka
Jaji alitoa hukumu baada ya ______________
(a) mabishano ya wanasheria (b) kumuona Mzee Mkenule
(c) Siku ya hukumu (d) wazee wa baraza
(e) Kumuondolea mashtaka Mzee Mkenule
SEHEMU E: UTUNGAJI
Zipange sentensi zifuatazo kwa kuzipa herufi A, B, C, D na E ili zilete habari yenye maana
Pale Rais wa nchi yetu alipotangaza kifo cha mpendwa wetu mzee Kawawa.
ilikuwa ni siku ya majonzi kwa watanzania wote.
Mzee huyu ameshawahi kushika nyadhifa mbalimbali nchini mwetu ikiwemo ya uwaziri mkuu.
Kamwe hatutasahau busara na uzalendo aliokuwa nao mzee Kawawa kwa nchi yetu.
Siku ya mwisho kabisa ya mwaka jana …